Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa hao mapema jana wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkaoni humo.
Aidha Amesema kuwa Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki na linatilia shaka utendaji kazi wao.
Hata hivyo, Majaliwa amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri zote nchini wabadilike na wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi kwa ushirikiano kwani wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.
