Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite katika migodi ya Mererani wameipokea kwa mabango kamati maalum ya bunge iliyoundwa na spika wa Bunge Job Ndugai kuchunguza mwenendo mzima wa madini ya Tanzanite ambapo baadhi ya mabango yamebeba ujumbe wa kuiomba serikali kuangalia upya sheria ya uchimbaji katika eneo hilo ili kupunguza migogoro baina ya wachimbaji wadogo na wakubwa.
Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wachimbaji hao wamepaaza sauti zao mbele ya kamati maalumu ya bunge ya kuchunguza mwenendo mzima wa madini ya tanzanite ambayo iko katika eneo hilo ikitekeleza baadhi ya majukumu yake ambapo ilipata nafasi ya kuzungumza na makundi yote muhimu kwa nyakati tofautitofauti.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Dotto Biteko analazimika kutoa ufafanuzi kidogo juu ya kazi na majukumu ya kamati hiyo huku akiwataka wachimbaji hao kuwa na subira mpaka pale kamati hiyo itakapokamilisha kazi yake ikiwemo kuandaa, kuchunguza na kutoa ushauri kwa serikali nini kifanyike dhidi ya kile ilicho kibaini baada ya uchunguzi wake.
Moja ya hadidu za rejea za kamati hiyo maalum ni kupitia mkataba uliopo baina ya shirika la taifa la madini STAMICO na Tanzanite One na kuangalia ushiriki wa Sky Associates ili kuona manufaa ambayo nchi inapata kutokana na biashara ya madini hayo.
