Kansela wa Austria Christian Kern amewahimiza washirika wa muungano wake wa kihafidhina kubakia serikalini baada ya kiongozi wa muungano huo kujiuzulu kwa ghafla, na kuongeza uwezekano wa kuitishwa uchaguzi wa mapema wakati chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kikiongoza katika uchunguzi wa maoni.
Uchaguzi mpya unaweza kukipa chama kinachopiga sera za uhamiaji cha Freedom Party – FPO nafasi ya kuingia katika serikali ya kitaifa ikiwa ni chini ya mwaka mmoja baada ya mgombea wake kushindwa katika kinyang’anyiro kikali cha urais.
Naibu wa Kansela Reinhold Mittelana, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha People’s Party – OVP alisema mapema jana kuwa anajiuzulu baada ya kushindwa kutuliza malumbano ndani ya chama na uvumi kuhusu uongozi wa usoni wa chama hicho.
Waziri wa Mambo ya Kigeni Sebastian Kurz ambaye ana umri wa miaka 30 huenda akachukua wadhifa huo.
Viongozi wa chama cha OVP watakutana Jumapili ijayo kumtafuta mrithi wa Mitterlehner
