Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,ametoa wito wa kubuniwa mkakati mpya wa maendeleo barani Afrika.
Amesema mataifa makubwa yalioendelea kiviwanda yanapaswa kuwa tayari zaidi kupeleka silaha kuyasaidia mataifa ya Kiafrika yanayopambana dhidi ya makundi ya wanamgambo.
Merkel pia ameisifu ujasiri wa mataifa ya Afrika ambayo yanashiriki katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali na mataifa jirani.
Ameongeza kuwa Ujerumani itaunga mkono juhudi za Ufaransa kulishinikiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha kikosi cha Afrika Magharibi kupambana na ugaidi na usafirishaji haramu wa binadamu katika eneo la Sahel.
Kiongozi huyo wa Ujerumani pia ametangaza mipango ya mapatano kati ya kundi la mataifa ya G20 na bara la Afrika, ambayo yanaondokana na mfumo wa zamani wa misaada ya kimaendeleo na badala yake kujikita katika fursa za ushirikiano na mataifa ya Afrika, ambayo mengi yanashuhudia viwango vikubwa vya ukuaji wa kiuchumi.
