KATAMBI AFURAISHWA USHIRIKISHWAJI WA WAZAWA MRADI WA SGR

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amefurahishwa na ushirikiwaji wa wazawa katika Mradi wa Reli ya Kisasa, ambao umeweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Amesema hayo baada ya kutembelea Mradi wa Reli ya Kisasa, maarufu SGR (Standard Gauge Railway) mkoani Tabora kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na masuala ya afya na usalama mahala pa kazi.

Mheshimiwa Katambi amesema kuwa, asilimia 90 ya manunuzi ya bidhaa na vifaa katika mradi huo yamekuwa yakifanyika ndani ya nchi kwa lengo la kutunza thamani ya fedha, kuongeza ajira na ukuaji wa uchumi.

“Niendelee kusisitiza suala la Local Content liendelee kuzingatiwa katika mradi huu. Pia malighafi ambazo si lazima zitoke nje ya nchi ni vyema zikanunuliwa hapa nchini ili kuwawezesha ukuaji wa uchumi wetu,” amesema

Ameongeza kuwa, mpango wa urithishaji wa ujuzi kwa wazawa utekelezwe ipasavyo ili wataalamu wanapomaliza muda wa kufanyakazi hapa nchini, wazawa waweze kufanya kazi hizo badala ya kuwaacha wataalamu hao wa kigeni kuendelea kuomba vibali vya ajira.

Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka wakandarasi wadogo pamoja na makampuni yanayotoa huduma katika mradi huo kuhakikisha wanatekeleza sheria ya ajira na mahusiano kazini.

“Wakati mwengine unakuta wafanyakazi wanamalalamiko yao juu ya wakandarasi wadogo au makampuni yanayotoa huduma katika mradi huu, lakini wakitoa taarifa ya changamoto zao wanalalamika kampuni ya Yapi Markezi au TRC wakijua ndio kampuni ambazo zimewaajiri kwa kuwa wanafanyakazi hapa. Uwepo utaratibu wa subcontractors hao wanatekeleza sheria ya ajira na mahusiano kazini,”

Pia, Naibu Waziri Katambi ametaka masuala ya afya na uslama mahala pa kazi kuendela kuzingatiwa wakati wote sambamba na kuhakikisha wafanyakazi wanavaa vifaa kinga muda wote wa kazi.

“Dhamira ya Serikali ni kuona mradi huu unakamilika bila kuleta madhara kwa wafanyakazi. Tutafanikisha hayo kama suala la afya na usalama katika maeneo ya kazi yatazingatiwa, hivyo hatutasita kuchukua hatua tukiona hayo hayatekelezwi,” amesema.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akizungumza na viongozi wa kampuni ya Yapi Markezi alipotembelea Mradi wa Reli ya Kisasa, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na masuala ya afya na usalama mahala pa kazi, Mkoani Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Louis Bura (kulia) akieleza jambo wakati wa ziara hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na masuala ya afya na usalama mahala pa kazi katika mradi wa Reli ya Kisasa Tabora – Isaka, Mkoani Tabora.
Naibu Meneja Mkuu wa kampuni ya Yapi Markezi (LOT 3 na LOT 4), Bw. Hakan Alkam akifafanua jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na masuala ya afya na usalama mahala pa kazi katika mradi huo, Mkoani Tabora.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (wa tatu kutoka kushoto) akizungumza na wafanyakazi wanaotoa huduma ya ulinzi katika ujenzi wa Reli ya Kisasa Tabora – Isaka, alipotembelea mradi huo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria za kazi na masuala ya afya na usalama mahala pa kazi, Mkoani Tabora.
Exit mobile version