Katibu Mkuu wa (CUF) afanya ziara kimya kimya Jijini Dar es salaam,kwa kutembelea wagonjwa na kutoa pole kwa wafiwa

   KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amefanya ziara kimya kimya jijini Dar es Salaam, kwa kutembelea wagonjwa na kutoa pole kwa wafiwa wa chama hicho.
Ziara hiyo ameifanya huku akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwamo Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea (CUF), Naibu Meya wa Jiji, Mussa Kafana na Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto.
Katibu mkuu huyo alifanya ziara hiyo katika kata za Gongolamboto, Majohe, Kigamboni na Upanga, ambapo alizungumza na wananchi mbalimbali aliowakuta katika maeneo husika kwa kuwataka kuwa watulivu, huku akiahidi changamoto zinazokikabili chama hicho zitamalizika hivi karibuni.
Mbali na hilo pia aliwaahidi wanachama wa chama hicho kujiandaa ,kuchukua ofisi yao Buguruni muda wowote kuanzia sasa kwani wamefikia katika hatua nzuri.
Ziara hiyo ya kimya kimya imekuja siku chache baada ya Jeshi la Polisi kuzuia wanachama wa chama hicho, waliokuwa wamehamasishwa na Mbunge wa Temeke kwenda kufanya usafi katika ofisi za CUF Buguruni, Aprili 30, mwaka huu.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilimzuia kwa Maalim Seif na wafuasi wake kufanya hivyo kwa maana ya kuweza kuhatarisha amani kwa wananchi iliyopo.
Exit mobile version