Kufuatia utafiti uliobaini uwepo wa mashapo ya madini aina ya Bunyu (grafait) tani 689.7 milioni katika mikoa ya Lindi na Mtwara, wananchi wa kata ya Chiwata wilayani Masasi mkoani Mtwara wanaozunguka mradi wa mgodi wa madini hayo wameiomba serikali kusimamia viwango vya malipo ya fidia kutokana na thamani ya ardhi na wanavyonufaika nayo.
Katika mkutano maalum wa hadhara uliotishwa na wananchi hao ulioshirikisha mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na kampuni ya utafiti ya Nachi Resources wameiomba serikali kuangalia upya viwango vya malipo ya uthamini wa ardhi yao iliyogundulika kuwa na madini ya grafait ambayo hutumika katika kutengeneza Betri zinazotumika katika magari, simu, tochi pamoja na kuzalisha penseli.
Kufuatia hali hiyo iliyotawala mkutano huo ikiwemo ujumbe wa mabango kutoka kwa wananchi ,Mbunge wa jimbo la Ndanda pamoja na mtafiti wa mradi huo kutoka kampuni ya Nachi Resources wamezungumzia madai ya wananchi hao na kutolea ufafanuzi.
Madini ya grafait ama bunyu yamegundulika katika vijiji vya chiwata na chidya katika mkoa wa Mtwara ambapo kwa mkoa wa lindi yamegundulika katika vijiji vya Chunyu, Mihewe, Matambalale, Chikwale, Namikulo, Chiundu, Nagulugai wilayani Ruangwa na kwenye kata ya Namangale wilayani humo.
