Kundi la Boko Haram linapanga kulipua bomu katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, amesema mtu mmoja anayesemekana kuwa ni mpiganaji wa kundi hilo ,la wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam, akizungumza katika mkanda wa video ulionekana na shirika la habari la Reuters.
Mtu huyo amesema katika vidio hiyo kwamba, mashambulizi zaidi ya mabomu yanapangwa , ikiwa ni pamoja na mjini Abuja ambako wananachi ndipo wanapojihisi wapo salama.
Ukanda huo wa vidio umepatikana na waandishi habari wa tovuti ya habari ya Sahara iliyoko Marekani wakishirikiana na mwandishi habari wa nchini Nigeria Ahmad Salkida.
Shirika la habari la Reuters hata hivyo halikuweza mara moja kuthibitisha ukweli wa video hiyo.
