Maambukizi ya virusi vya corona yapungua China.

Kasi ya maambukizi ya virusi vya corona imepungua nchini China, lakini idadi ya maambukizi ya ugonjwa huo unaofahamika kama COVID-19 yamepanda kimataifa na kufikia watu 90,000. Huku kukiwa na zaidi ya visa 2,100 vilivyothibitishwa katika Umoja wa Ulaya, jumuiya hiyo imeongeza kiwango cha kitisho cha virusi hivyo kutoka “cha chini hadi cha wastani” na kukifanya kuwa “cha wastani hadi cha juu.” Italia, ambayo ndiyo nchi iliyoathirika pakubwa barani Ulaya sasa ina zaidi ya visa 2,000, huku watu 52 wakithibitishwa kufa. Idadi ya vifo nchini Marekani imepanda hadi watu sita. Barani Afrika, visa vya kwanza vya virusi hivyo vimeripotiwa Morocco, Tunisia na Senegal. Mawaziri wa fedha kutoka nchi za kundi la G7 wanapanga kuandaa kongamano leo kujadili hatua za kukabiliana na kuongezeka kwa athari ya kiuchumi kutokana na mripuko huo. Shirika la Biashara Duniani – WTO limeonya kuwa janga hilo lina athari kubwa kwa biashara.

Exit mobile version