Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema leo kuwa janga la virusi vya corona limesababisha kuanguka kwa hali ya Haki za Binadamu duniani .
Akizungumza wakati wa mjadala ndani ya bunge la shirikisho mjini Berlin, Maas amesema ulimwengu unashuhudia jinsi mzozo wa COVID-19 unavyowaimarisha watawala wanaotumia mabavu.
Maas ameorodhesha hatua za ukandamizaji zilizochukuliwa dhidi ya waandishi habari nchini Urusi, Venezuela, Iran, Uturuki na China kama mifano ya matumizi ya nguvu katika kushughulikia kadhia ya Corona.
Mwanasiasa huyo wa chama cha SPD pia amegusia namna baadhi ya mataifa ya Ulaya ikiwemo Hungary yanavyotumia vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona kudhoofisha utawala wa sheria.