Maaskofu wa kanisa la Anglikana kutoka dayosisi 28 Tanzania bara na visiwani wamekutana jijini Arusha na kutoa tamko la kuunga mkono jitihada zote za serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Akitoa tamko hilo leo jijini Arusha Askofu Mkuu wa kanisa Anglikana Tanzania,ambaye pia ni Askofu wa dayosisi ya Tanga,Askofu Dokta Maimbo Mndolwa alisema kuwa,kama kanisa wamejipanga kuendelea kuunga mkono jitihada zote za serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na wananchi na waumini wa kanisa hilo.
Askofu Mndolwa alisema kuwa,kanisa hilo katika kupambana na ugonjwa huo wanaendelea kufanya maombi ya mara kwa mara katika dayosisi zote ,jumuiya na familia kwa ajili ya kumwomba Mungu kutuepusha na ugonjwa huo usiendelee kusambaa zaidi hapa nchini.
Alisema kuwa,wanaishauri serikali kuhimiza vyombo vya usafiri kuchukua hatua za tahadhari ikiwemo kusafisha mabasi,ndege na maeneo ya usafiri .
“Tunaomba serikali kusimamia mfumuko wa bei katika bidhaa muhimu na vyakula katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huo wa Korona.””alisema Askofu.
Askofu Mndolwa alisema kuwa,wao kama.kanisa wana imani kubwa kuwa hakuna lisilowezekana kwa Mungu ,hivyo wanaendelea kupiga magoti kutafuta uso wa Mungu katika kipindi hiki Cha kwaresma ili asikie Sala zetu na kuturehemu.
Alisema kuwa ,kanisa linaelekeza kuwa kila dayosisi itenge siku maalumu ya maombi kuanzia machi 19 kwa ajili ya kuombea ugonjwa huo ili Mungu aweze kuingilia Kati.
Askofu aliongeza kuwa ,kama kanisa kwa pamoja siku ya ijumaa kuu itakuwa siku ya ibada ya pamoja kanisa la Anglikana Tanzania kwa ajili ya kuombea Taifa letu dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona
“Tutaendelea kuwaombea wafanyakazi wote wanaotoa huduma kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Corona ili Mungu awaepushe na magonjwa hayo sambamba na kuwapa uvumilivu katika kuwahudumia .”alisema Askofu
Aidha ugonjwa huo ulianzia nchini China desemba 2019 na kuenea sehemu mbalimbali hapa duniani,ambapo mpaka sasa hivi kwa Tanzania kuna wagonjwa watatu wenye maambukizi ya virusi vya Corona