Majaji wa Mahakama ya Juu wameanza kuandika uamuzi wa kesi ya kupinga ushindi wa rais Uhuru Kenyatta, iliyowasilishwa na kiongozi wa Muungano wa upinzani NASA Raila Odinga.
Hatua hii inakuja baada ya Majaji hao kutamatisha kibarua cha kusikiliza Mawakili wa upande wa Tume ya uchaguzi, wale wanaomwakilisha rais Kenyatta na wale wa muungano wa upinzani NASA.
Mawakili wa NASA, wakiongozwa na James Orengo, wanataka Mahakama hiyo kutupilia mbali kesi hiyo baada ya kuonesha kuwa kulikuwa na ushahidi mkubwa, Uchaguzi huo haukuwa huru na haki.
Akitoa ripoti ya mwisho, Orengo alisema ikiwa Mahakama hiyo itaangalia kikamilifu ushahidi wote uliowasilishwa, basi ushindi huo utatupiliwa mbali.
Paul Muite anayewakilisha Tume ya Uchaguzi katika kesi hiyo alisema kuwa, pamoja na kwamba huenda kulikuwa na dosari ndogondogo, zoezi hilo lilikwenda vizuri.
