Makamu Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay

Chama cha wamiliki wa malori chajitosa, chadai makubaliano yaliyofikiwa yamekiukwa, chaiomba Serikali kuingia kati

CHAMA cha Wamilikiwa Malori Tanzania (TATOA) kimeiomba Serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na nchi jirani ili kutatua changamoto ya madereva wa malori nchini kunyanyasaka mpakani katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona.

Ombi hilo la TATOA limekuja baada ya makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Kenya yaliyokuwa yamefikiwa hivi karibuni ikiwemo madereva waliopewa cheti ya kupimwa Corona kuruhusiwa kupita mpakani na kuingia nchi jirani kwa ajili ya kupeleka na kushusha mizigo.

TATOA imesema pamoja na makubaliano yaliyofiwa baina ya Kenya na Tanzania,lakini bado kumekuwa na changamoto za kukataliwa kwa vyeti hivyo, hivyo kuzuiwa mpakani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Elias Lukumay, amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo madereva wa Tanzania ni pamoja unyanyasaji na unyanyapaa unaofanyika katika mpaka wa Rusumo unaounganisha Tanzania na Rwanda na mpaka wa Namanga wanapotaka kuingia Kenya.

Amesema licha ya kuwepo kwa makubaliano yaliyofikiwa, lakini bado kuna mambo yameendelea kujitokeza na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana.

Lukumay amesema wapo madereva wamekaa muda mrefu katika mpaka wa Rusumo wakisubiri kushusha mizigo yao na wengine wakisubiri kuvuka kwenda nchi ya Congo .

“Madereva hao wamekuwepo hapo kwa muda katika eneo la Galina ambalo halina huduma toshelezi za kijamii kulingana na idadi kubwa ya madereva wanasubiri kuvuka na hata wale wanaovuka kuingia Rwanda kwa utaratibu uliowekwa wa kusindikizwa, lakini bado wanapitia katika mazingira magumu ya kukosa huduma za kijamiii,” amesema na kuongeza;

“Katika kipindi hiki bado hakuna usawa wa ufanyaji biashara kwani kwa sasa magari ya Tanzania yanatakiwa kuishia mpakani isipokuwa kwa yale yaliyobeba mizigo iliyoainishwa kama bidhaa muhimu, wakati huo huo magari za Rwanda  yanaruhusiwa kusafiri zaidi ya kilometa 1,000 kuja Dar es Salaam kuchukua mizigo bila madereva kubugudhiwa na kupeleka mizigo hiyo hadi mlangoni kwa wateja,” amesema Lukumay

Aidha amesema utaratibu huo umesababisha waagizaji wa mizigo kupendelea zaidi kutumia magari ya Rwanda kwani yamekuwa yakifikisha mizigo ya wateja hadi milangoni, huku magari ya Tanzania kuishia mpakani hivyo kufanya mazingira ya biashara kutokuwa ba usawa kwa pande mbili.

Lukumay amesema gharama za ufanyaji biashara nazo zimeongezeka kwani eneo lililotengwa na Serikali ya Rwanda lina miundombinu hafifu ya ushushaji, uhudumiaji na uhifadi wa mizigo hivyo kusababisha magari ya Tanzania kusubiri muda mrefu hadi pale magari ya Rwanda yanapopatikana kufaulisha mizigo.

“Ucheleweshaji huo wa magari unasababisha wasafirishaji wa Tanzania kuendelea kutozwa faini za makontena hadi kiasi cha sh.120,000 kwa siku,” amesema.

Akizungumzia vyeti vya vipimo vya ugonjwa wa Corona kwa madereva,Lukumay amesema makubaliano yaliyofikiwa na nchi ya Kenya ni madereva kupima na kupata cheti ambacho kingekubalika pande zote na kumuwezesha deareva kuvuka bila kikwazo.

Amesema pamoja na makubaliano nayo mamlaka ya Kenya zimebadili tena mwelekeo ghafla na kuvikataa vyeti hivyo bila kuwepo kwa makubaliano yeyote.

“Hali ya kukataa vyeti hivyo imesababisha madereva kupata tabu katika mpaka wa Namanga na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara hasa wanaosafirisha bidhaa zinazoharibika kwa haraka,” amesema Lukumay.

semiosonyo5

Kitaifa

Exit mobile version