MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za kifedha za nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) kufahamu kuwa utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi kamwe hauwezi kuzisaidia nchi masikini kuondoka kwenye hali hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kufungua mkutano wa taasisi za fedha kutoka nchi za SADC, Samia amesema kwa sasa nchi hizo zinatakiwa kuongeza juhudi za kuweka mikakati itakayohakikisha raslimali za ndani ya nchi, husika zinachangia kikamilifu kukuza uchumi wa nchi na kukuza sekta binafsi.
Ametoa Mwito kwa Taasisi za Maendeleo za Kifedha kuhakikisha kuwa zinashiriki kikamilifu katika kuiwezesha kifedha miradi mbalimbali ya kimaendeleo, kama ujenzi wa miundombinu ambako benki nyingi zimekuwa zinakwepa.
Samia pia amesema ufadhili wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika nchi mbalimbali kwa sasa unafanywa kwa kasi kubwa kwa fedha za nje pamoja na fedha za ndani kupitia taasisi za kifedha za nchi husika.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashati Kijaji amesema mkutano huo ambao unazikutanisha taasisi 37 za kifedha za SADC, kutoka nchi 14 zinafanya mkutano wa mwaka hapa nchini huku kauli mbiu yao ni mkakati wa maendeleo ya viwada kwa maendeleo endelevu.
Amesema hata msisitizo katika bajeti iliyopitishwa hivi karibuni ni viwanda na akaeleza kuwa mkutano huo ni muhimu kwani hakuna viwanda kama hakuna fedha. Alisema kwa sasa nchi za SADC zinahitaji kutumia rasilimali za ndani badala ya kutegemea fedha za nje.
