Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, amesema Taifa halipo tayari hata kidogo kupokea misaada yenye masharti ambayo haiendani na mila na desturi za Kitanzania.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson pamoja na Mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel, Craca Machel pamoja na ujumbe walioambatana nao Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuna baadhi ya wafadhili wanaisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na bila masharti mabaya lakini kuna baadhi ya wafadhili wanaonyesha wazi kuwawanataka Serikali ikubali masharti yao.
Amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali itaendelea kusimamia maadili ya Taifa ipasavyo na imeweka mipango na mikakati mizuri kwa ajili ya kuongeza mapato yake ya ndani ili kuondokana na utegemezi kutoka kwa baadhi ya wafadhili ambao wanaahidi kuchangia bajeti kuu ya Serikali lakini mwisho hawafanyi hivyo.
