Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa chakula, kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula kutoka serikalini.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Musoma ,katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini humo.
Samia amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa mvua, au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine ,na sio kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema ya chakula kutoka kwa Serikali.
Amewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo, na pindi wanapovuka wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuna, ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Pia aliwataka viongozi wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
