Naibu Waziri wa Fedha Dk. Ashantu kijaji amesema ifikapo Julai 30 waajiri wote ambao hawajapeleka michango au kumalizia michango ya wafanyakazi wao watachukuliwa hatua za kisheria zikiwemo kuwafikisha mahakamani wale wote watakaopuuza agizo hilo.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa mwaka wa wadau wa Mfuko wa Mafao ya kustaafu (GEPF), jijini Arusha ,dakta kijaji amesema kushindwa kuwasilishwa michango ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini kwa wakati kunakofanywa na baadhi ya waajiri kunatia mashaka utendaji wa Bodi za mifuko.
Dk. Kijaji alihoji kigugumizi kinachofanywa na Bodi za Mifuko ya Jamii kushindwa kutekeleza wajibu halali wa kisheria kwa waajiri wote wasiowasilisha michango ya waajiriwa wao.
Aidha, aliitaka mifuko hiyo nchini kupitia Jumuia ya Mifuko hiyo nchini (TSSA), kuhakikisha wanazingatia misingi ya uwekezaji wa viwanda vyenye tija utakaozingatia uzalishaji faida, kuleta ajira na mwisho kumlipa mwanachama mafao yake kwa wakati pale anapostahili.
Mwenyekiti wa Bodi ya GEPF Joyce Shaidi amesema, mfuko huo kwa sasa umepitia upya mkakati wa uendeshaji wa mfuko huo ukilenga ifikapo Juni, Mwaka 2020 mfuko huo uwe na thamani ya Sh.Trilioni 1.
Mkutano huo wa siku mbili umeshirikisha wadau wote wa mfuko huo ambao kauli mbiu yake ni hifadhi ya jamii kwa wote inawezekana katika uchumi wa viwanda pia watazindua mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi na mtu mmoja mmoja katika sekta isiyo rasmi kwa wanachama wa mpango wa hiyari.
