Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza Makatibu Mahususi nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na waache tabia ya kutoa siri za ofisi zao kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Bi Samia ametoa kauli hiyo wakati anafungua mkutano wa Tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Mji Dodoma.
Samia amesema uadilifu na uaminifu ni njia pekee ya kuaminiwa na viongozi wao hivyo ni muhimu kwa makatibu mahsusi nchini kufanya kazi kwa bidii na ubunifu mkubwa katika maeneo yao ya kazi.
Bi Samia pia amewahimiza makatibu mahsusi kufanya tathmini ya utendaji wao wa kazi na wawe tayari katika kujifunza mbinu mpya za utendaji zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki amesema Serikali inafanyia kazi baadhi ya kero zinazowakabili makatibu mahsusi ikiwemo kuboresha maslahi ya kada ya uhazili nchini.
