Serikali imezihimiza Mamlaka za maji na mabonde ya maji kubuni vyanzo vipya vya mapato, vitakavyosaidia kujiendesha vyenyewe bila kutegemea serikali kuu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alipokuwa akizungumza na watumishi wa mamlaka ya maji Singida (SUWASA), Bonde la maji kanda ya kati na Maabara .
Amesema kuwa Serikali haina fedha za kukidhi mahitaji yote ya mamlaka za maji na mabonde nchini, hivyo ni vyema vikaweka mikakati ya kujitengemea kimapato.
Aidha, Katibu Mkuu amewataka watumishi wa SUWASA, kutoa huduma bora itakayovutia wananchi wengi zaidi kupata huduma ya maji katika mamlaka hiyo.
Hata hivyo, Katika hatua nyingine, Prof. Mkumbo ametumia nafasi hiyo kusisitiza utaratibu wa kulipia kwanza maji (pree paid), kabla ya kupata huduma ya maji.
Kwa upande wake Afisa Maji bonde la kati, Benard Chikarabhani amesema kuwa wameanza utekelezaji wa ujenzi wa bwawa la Farkwa, kwa lengo la kuongeza usambazaji wa maji katika mji wa Dodoma, Bahi, Chamwino na halmashauri ya wilaya Chemba.
