Mfanyabiashara Yusuf Manji ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo kuwa, yeye bado ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu.
Manji amedai kuwa hatambui kuvuliwa udiwani kama ilivyotangazwa na Mstahiki Meya wa Temeke Abdallah Chaulembo September 6 mwaka huu.
Manji ametoa malalamiko hayo kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.
Katika kesi hiyo ambayo Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, amedai upelelezi haujakamilika na Manji kudai ameona habari kupitia gazetini kuwa amevuliwa udiwani.
Amedai kama ni kweli amevuliwa Udiwani hatambui, kwani ana miezi 2 yupo gerezani na serikali inatambua kwamba yeye ni Diwani.
Pia Manji amedai kama hilo haliwezekani, basi wamuandikie barua itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua pia.
Aidha amedai hiyo kesi ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande wake wa kesi tu, kwani yeye amechaguliwa na wananchi na anawasaidia.
Awali kabla ya kuelezwa hayo Wakili wa utetezi Seni Malimi, alidai wanatarajia kuwasilisha maombi ambayo ni ya siri katika tarehe ijayo.
Baada ya kuelezwa hayo Hakimu Huruma Shaidi akautaka upande wa mashtaka kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo, ambapo kesi imeahirishwa hadi September 18 mwaka huu.
