Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani inachunguza ripoti za matukio ya kushangaza ambayo yamewaathiri Wamarekani 16 wanaoishi Cuba.
Ripoti kadhaa za vyombo vya habari zimedokeza kuwa huenda walikuwa waathiriwa wa kile kinachifahamika kama “shambulizi la kutumia kifaa cha sauti”.
Maafisa wanasema raia wa Marekani wanaofanya kazi katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Havana wamekumbwa na dalili za kimwili zinazosababishwa na “matukio” yasiyotambulika ambayo yalianza mwishoni mwa mwaka wa 2016.
Wafanyakazi kadhaa walirejeshwa nyumbani Marekani kutokana na matatizo ya kusikia na madhara mengine. Kwa mujibu wa televisheni ya CBS, madhara hayo ni pamoja na kichefuchefu, matatizo ya kutoweza kusimama vizuri na hata kuumia kwa ubongo.
