Marekani yaiwekea vikwazo benki moja ya China

China imeghadhabishwa sana na hatua ya Marekani ya kuiwekea vikwazo benki moja ya China ambayo inatuhumuwa kuhusika katika utakatishaji wa fedha za Korea Kaskazini.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo ameitaka Marekani “kukoma kuchukua hatua zisizo sahihi” kuepusha kudhuru ushirikiano baina ya nchi hizo.
Marekani ilitangaza hatua hiyo, pamoja na vikwazo dhidi ya kampuni ya uchukuzi wa meli ya China na raia wawili wa China mnamo Alhamisi.
Imesema lengo la vikwazo hivyo ni kupunguza fedha ambazo Korea Kaskazini ,inaweza kutumia kuendeleza mpango wake wa kustawisha silaha.
Umoja wa Mataifa ulikuwa tayari umeiwekea Korea Kaskazini msururu wa vikwazo, lakini China inatazamwa na wengi kama taifa lililo na uwezo zaidi wa kuiyumbisha Korea Kaskazini kupitia vikwazo vya kiuchumi.
Washington imekuwa ikiishinikiza Beijing kuchukua hatua kali zaidi hasa kutokana na hatua ya Pyongyang ya kufanyia majaribio makombora ya masafa marefu.
Lakini kupitia Twitter mapema mwezi huu, Rais Donald Trump amesema hatua ambazo China imechukua kufikia sasa hazijatosha.
Exit mobile version