Masaa 4 ya mahojiano ya Lowassa na DCI haya hapa.

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amehojiwa kwa zaidi ya saa 4 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa tuhuma za uchochezi.

Lowassa amehojiwa jana Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Polisi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8:14 mchana, kwa kile alichodai kuwa ni kutokana na hotuba aliyoitoa Jumamosi katika Jimbo la Ukonga lililo chini ya Mbunge, Mwita Waitara.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mahojiano hayo, Lowassa amesema kuwa baada ya mahojiano hayo, anatakiwa kuripoti tena katika ofisi hizo kesho saa 6 mchana.

Aidha, amesema kuwa wapo katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kwamba wanachama wake wawe na amani, kwani mambo yako safi na ameitwa kwa nia njema.

Wakili wa Lowassa, Peter Kibatala amesema walipokea mwito kutoka kwa DCI ukimtaka aripoti saa 4 jana ambapo ameeleza kuwa Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya kichochezi Juni 23, mwaka huu katika futari iliyoandaliwa na Waitara.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema walioruhusiwa kuingia ndani kwenye mahojiano ni Lowassa na wanasheria wake na kwamba wao walikuwa nje kama watazamaji.

 

Exit mobile version