MASHIRIKA manne ya kimataifa kwa pamoja jana yalielezea kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya usafi ijulikanayo kama Niko Tayari inayoendeshwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mashirika hayo ni UNICEF (Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto), Benki ya Dunia, Shirika la misaada la Uingereza (DFID), Shirika la Miradi la Ujerumani (GIZ) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).
Mashirika hayo ya maendeleo ambayo wawakilishi wake walikutana jana jijini Dar es Salaam, yamekubali kuunga mkono kampeni hiyo iliyozinduliwa mwezi uliopita mjini Dodoma. Kampeni hiyo imelenga kuhamasisha usafi wa mazingira kwa kila Mtanzania hasa kuwa na choo katika kila familia na kujenga utamaduni wa kunawa mikono.
Akizungumza jana, Mratibu wa kampeni ya Nipo Tayari, Anyitike Mwakitalima kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema ili kuwa na huduma bora ya maji, usafi wa mazingira ni muhimu kuzingatiwa.
Kampeni hiyo ya usafi wa mazingira na matumizi bora ya choo (NikoTayari) inatarajiwa kuwa chachu ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuboresha afya za Watanzania wote, mijini na vijijini.
