Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Mauritius nchini Tanzania Mhe. Jean Pierre Jhumun mwenye makazi yake mjini Maputo,Msumbiji aliyeongozana na Wawekezaji wa Uzalishaji Sukari ambao wameonyesha nia na utayari wa kuwekeza nchini.
Hata hivyo Mbali wa ujumbe kutoka Mauritius, wengine waliohudhuria mazungumzo hayo ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Profesa Godius Kahyarara naMkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF , Bw .William Erio .
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji hao ushirikiano wa Serikali na kuwaeleza kuwa Tanzania ina mazingira bora ya uwekezaji, Mbali ya fursa ya uwekezaji katika Sukari, Makamu wa Rais aliainisha maeneo mengine ya kuwekeza kama vile viwanda na TEHAMA.
Aidha amesema pindi uwekezaji huo ukifanikiwa , Tanzania itafaidika na soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na masoko mengine duniani kwa ujumla.
