Mbaroni kwa kumua Mpenzi wake

JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam linamshikilia Musuguri Sylvester (29), mkazi wa Sinza, kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake, kisa wivu wa mapenzi.

Hayo yalisemwa jijini hapa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kamanda Sirro alisema tukio hilo lilitokea Machi 31, mwaka huu saa saa nne usiku katika maeneo ya Sinza Shekilango jijini Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya ufuatiliaji wa taarifa ya tukio la mauaji ya mwanamke aliyejulikana kwa jina la Samira Masoud (34) aliyeuawa kwa kuchinjwa Machi 7, huko Kibamba na kisha mwili wake kuwekwa katika jaba la maji huku ukiwa umeharibika vibaya.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo katika mahojiano, amekiri kufanya mauaji ya mwanamke huyo na kusema sababu kubwa ilikuwa ni wivu wa kimapenzi baada ya kumfumania mpenzi wake akiwa chumbani na mwanamume mwingine ambaye hata hivyo mwanamume huyo alitoroka.

Alisema awali mtuhumiwa huyo aliwatumia ndugu wa marehemu ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutumia namba ya simu ya marehemu ukisema: “Nendeni mkachukue maiti ya ndugu yenu itaozea ndani.”

“Mtaweza kuona ni ukatili wa namna gani uliofanywa na kijana huyu, hata kama mtu umemshika ugoni hupaswi kufanya tukio kama hili la kinyama,” alisema Kamanda Sirro na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Chanzo:Habari Leo

Exit mobile version