KITUO cha Utafiti wa Kilimo Selian mkoani Arusha kimepata mbegu bora aina tatu za maharage yenye sifa ya usindikaji, ikiwa ni mkakati wa kuwaandaa wakulima wa zao hilo kuwa na mbegu zitakazofaa kwenye viwanda vya usindikaji.
Mtafiti Kiongozi wa zao hilo kituoni hapo, Papias Binangwa amesema watafiti wanafanya jitihada hizo ,ili wakulima wachangamkie fursa za viwanda vinavyohimizwa na serikali ya awamu ya tano.
Amesema kituo hicho kimetafiti na kufanikiwa kupata mbegu tatu ambazo ni SWP -9, SWP – 10 na SWP – 11, tayari kimekamilisha taratibu za kiutafiti na kuzipeleka kwenye Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) kwa ajili ya kuomba kibali ili kuipitisha kuwa mbegu na kutumika kwa wakulima.
Binangwa amesema si kila maharage yanayolimwa na wakulima yanafaa kusindikwa na kuuzwa kwenye maduka makubwa na madogo,kwenye makopo bali kuna sifa zinazotakiwa kuonekana kwenye maharage yanayosindikwa, hivyo aina hizo zina sifa ya usindikwaji kwa asilimia 90.
Amesema pamoja na kuwa na sifa za usindikwaji kwa mbegu hizo aina tatu walizozipata lakini pia zina uwezo wa kuzalisha wastani wa tani mbili kwa hekta kutegemea na matunzo ya shamba ya mkulima hususani matumizi ya kilimo bora cha zao hilo.
Amesema hivi sasa katika maduka makubwa ya kuuzia chakula, kuna maharage kutoka nje ya nchi kwa kuwa hapa nchini hapakuwepo na aina bora zenye sifa ya usindikaji.
