Kamati ya Haki,Maadili na Madaraka ya Bunge imemsimamisha Mbunge wa Viti Maalum Conchesta Rwamlaza kuhudhuria vikao vitatu vya Bunge kuanzia Siku ya Jana kwa kosa la kusema uongo bungeni.
Akichangia Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 RWAMLAZA, amesema Mbunge wa Muleba profesa ANNA TIBAIJUKA akiwa waziri wa wizara hiyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kujilimbikizia ardhi zaidi ya hekari 4,000.
Aidha Kamati hiyo imemsamehe Mbunge wa Arumeru Mashariki JOSHUA NASSARI ambaye mwaka jana, katika mkutano wa tatu alidharau mamlaka ya Spika na kufanya fujo baada ya Mbunge wa Chemba JUMA NKAMIA kuomba mwongozo ,akitaka kujua ni kwa nini serikali imewafukuza wanafunzi wa Diploma maalum ya Sayansi katika chuo kikuu cha Dodoma(UDOM).
Akiwasilisha maamuzi ya kamati hiyo bungeni Mjini Dodoma Mwenyekiti wa kamati hiyo GEORGE MKUCHIKA, amesema wabunge wote wawili walifika mbele ya kamati na kusomewa tuhuma zao na kujieleza ambapo kamati ilijiridhisha na kutoa adhabu hiyo kwa RWAMLAZA, huku ikimsamehe NASSARI baada ya kukiri na kuomba radhi.
Katika hatua nyingine bunge limepitisha azimio la makataba wa Kimataifa wa kazi za Ubaharia wa Shirika la kazi Duniani ILO wa mwaka 2016, na Azimio la Mkataba wa Kimataifa wa vitambulisho vya mabaharia namba 185 wa mwaka 2003 wa ILO.
