Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi, amewasilisha kwenye Kamati Maalumu ya Bunge miswada miwili, huku akisisitiza wajumbe kujadili kwa manufaa ya taifa na si maslahi binafsi.
Miswada iliyowasilishwa jana ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi, na ule wa Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.
Aidha, kamati leo zitaanza kukutana na wadau wa madini ili kukusanya maoni kabla ya muswada huo kujadiliwa na bunge katika vikao.
Akiwasilisha muswada wa pili wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi, Profesa Kabudi amesema mikataba hiyo haiendi kinyume na Katiba na ya misingi ya sheria za kimataifa kwa sababu Tanzania ni sehemu ya dunia.
Kabudi amesema kwa mujibu wa masharti yaliyopendekezwa baada ya kubaini kuna masharti hasi katika mikataba hiyo, Bunge linaweza kuitaka serikali kufanya majadiliano upya na upande wa pili wa mkataba ili kuondoa masharti hayo.
Aidha, Muswada huo unakusudia kutekeleza masharti ya Ibara ya 27 ya Katiba, ambayo pamoja na mambo mengine, inamtaka kila Mtanzania kulinda na kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
