Rais John Magufuli amesema amedhamiria kwa dhati kuleta maendeleo nchini, kupitia uwekezaji na uzalishaji mali katika uchumi wa viwanda,na pia amedhamiria kuufungua kiuchumi Mkoa wa Tanga.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanafanya kwa bidii shughuli za uzalishaji mali ikiwemo mboga vyakula na matunda, ili kukidhi mahitaji ya soko, litakalotokana na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani jijini Tanga, ambako kesho ataweka jiwe la msingi na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti akiwa katika miji ya Mkata, Komkonga, Kabuku, Hale, Muheza na Mkanyageni katika wilaya za Handeni, Korogwe na Muheza, alipozungumza na wananchi wakati alipowasili mkoani Tanga kuanza ziara yake ya kikazi.
Dk Magufuli amesema pamoja na ziara hiyo, ataweka jiwe la uzinduzi wa mradi wa bomba la mafuta Chongoleani jijini Tanga.
Amesema mradi huo utafungua fursa za kiuchumi mkoani huko na kuwataka wananchi kuchangamkia.
