Tume ya Uchaguzi Kenya imeahirisha mkutano ambao ulikuwa umepangwa kufanyika leo, kati ya mwenyekiti wa tume hiyo na wagombea wa urais.
Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kufanyika saa nane na nusu adhuhuri, lakini tume hiyo imetoa taarifa na kusema umeahirishwa.
Uchaguzi mpya wa marudio nchini Kenya umepangiwa kufanyika siku ya Alhamisi wiki ijayo tarehe 26 mwezi huu.
Ingawa Rais Uhuru Kenyatta amesisitiza yuko tayari kwa uchaguzi huo na utaendelea, mgombea wa upinzani Raila Odinga alijiondoa wiki iliyopita.
Jana Bw Raila Odinga ambaye ni mgombea wa muungano wa National Super Alliance Nasa, alitangaza siku hiyo badala ya kushiriki uchaguzi, wafuasi wake watafanya maandamano makubwa kote nchini humo.
