MKUU wa Mkoa wa Mbeya ameagiza Mkandarasi anayekarabati kipande cha barabara ya Tanzania na Zambia,TANZAM katika eneo la Simike jijini Mbeya kukamilisha kazi hiyo ndani ya juma moja , baada ya mradi huo kucheleweshwa kwa miezi sita, huku mkuu huyo wa mkoa akisema kuna umuhimu wa kuwepo kwa barabara mbadala za mzunguko jijini Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makalla ametoa agizo hilo wakati wa ukaguzi wa kushtukiza ambao ameufanya baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na msongamano wa magari kwenye eneo hilo.
Awali Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya TANROADS amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa barabara hiyo imechelewa kutokana na changamoto mbalimbali ambayo ni pamoja na aiana ya lami inayotumika.
Mradi wa matengenezo ya kipande hicho cha barabara chenye urefu wa kilomita 1.7, unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.061,na ulisainiwa Mwezi Aprili mwaka jana na kuanza kazi mwezi Juni ,ambapo muda wa utekelezaji ni miezi tisa na ulitakiwa kumalizika machi 31 mwaka huu.
