Waziri wa Ujenzi Atoa siku saba kwa kampuni ya reli Tanzania TRL kukarabati daraja la reli la Ruvu.

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Professa Makame Mbarawa ametoa siku saba kwa Kampuni ya Reli Tanzania TRL, kukamilisha ukarabati wa daraja la Reli la Ruvu lililoharibiwa na kukatika hivi karibuni kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kusababisha huduma za usafirishaji abiria na mizigo kusimama.

Waziri Mbarawa amesema hayo jana alipotembelea daraja hilo kwa lengo la kukagua na kuona maendeleo ya Ujenzi wa daraja la Ruvu ambao umekwisha anza na kusisitiza kuharakishwa ukamilikaji wa ujenzi huo ili kuruhusu huduma mbalimbali za usafirishaji kutoka ndani na nje ya nchi ambazo zimekwama kwa muda.

Aidha Waziri Profesa Mbarawa amesema kwa sasa Serikali ina mpango wa kudumu wa kuhakikisha madaraja yote ya reli nchini yanafanyiwa ukarabati wa kudumu ili kuhakikisha changamoto na athari za uharibifu wa miundombinu ya reli unaotokana na athari za mvua hazijitokezi tena huku akitaja mchakato uliopo sasa wa uanzishwaji wa Reli ya kisasa ambao utachangia kwa kiasi kikubwa kuondosha matatizo ya uharibifu wa madaraja ya Reli.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania TRL na Kampuni Hodhi ya Miundombinu na Rasilimali za Reli Masanja Kadogosa amesema Kampuni hiyo itatekeleza agizo hilo la Waziri Mbarawa kwa wakati kutokana na usafiri huo wa reli kuwa tegemeo la wananchi wengi , huku akitaja gharama zitakazotumika katika ujenzi wa Daraja hilo kuwa ni shilingi milioni 328 za kitanzania.

 

Exit mobile version