Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga amewataka watendaji wa Halmashauri ya Bariadi Mjini na Vijijini kuhakikisha fedha zote za makusanyo ya ndani zinazokusanywa na kikosi kazi zinaingizwa kwenye akaunti sahihi kabla ya kufanyiwa matumizi ya aina yoyote ili kudhibiti matumizi yasiyorasmi na unadhirifu wa fedha za umma.
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa agizo hilo katika kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika mjini Bariadi, ambapo amesema Serikali wilayani humo kupitia kamati ya ulinzi na usalama ilibani kusua sua kwa ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri hizo, hivyo kushauri kuundwa kikosi kazi ili kukusanya mapato ya ndani na jambo ambalo limeleta faida na kufikia lengo la makusanyo katika mwaka 2017.
Katika hatua nyingine Kiswaga amewataka wanunuzi wote wa zao la pamba kuhakikisha wanalipa madeni yao yote ya ushuru wa pamba katika Halmashauri hizo, kwani vinginevyo hawataruhusiwa kununua wala kupatiwa leseni za kununua pamba wilayani Bariadi.
