Wakuu wa nchi kutoka jumuiya ya umoja wa Ulaya wanatarajia kuonesha mshikamano wao wakati wa mkutano wao Jumamosi hii ambapo wataidhinisha mpango wa maelekezo ya miaka miwili kwa nchi ya Uingereza kujitoa kwenye umoja huo.
Wakuu hao kutoka nchi 27 zilizosalia wanatarajiwa kuitaka Uingereza kutatua masuala muhimu kuhusu kujitoa kwake kunakohusu watu, fedha na Jamhuri ya Ireland kabla ya kufanyika kwa mazungumzo yoyote ya baadae.
Mkutano huu unafanyika huku joto la kujitoa kwa Uingereza likiwa linapanda pamoja na vita ya meneno kati ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuhusu majadiliano.
Viongozi hao pia wanatarajia kuunga mkono wazo wa nchi ya Ireland Kaskazini kuwa mwanachama wa umoja huo ikiwa itaungana na Ireland na kuitaka Uhispania kuwa na usemi kuhusu athari za eneo la Gibraltar.
