Wizara ya Maliasili na utalii imewataka wadau wa uhifadhi kote nchini kuunga mkono mpango wa Serikali wa kujenga mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme, katika mto Rufiji kwenye pori la Akiba la Selous ambao ukikamilika unatarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,100.
Katibu Mkuu wizara ya Maliasili na utalii Meja Jenerali Gaudance Milanzi amesema utekelezaji wa mradi huo wa umeme, ni muhimu kwa taifa kwani utasaidia kuharakisha maendeleo ya taifa kuelekea azima yake ya Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Akiongea wakati akifunga mafunzo ya askari wa wanyamapaori kutoka Mamlaka ya wanayamapori Tanzania -TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Katibu mkuu Meja Jenerali Gudance Milanzi amesema mradi huo wa umeme, pamoja na mradi wa bwawa la maji la Kidunda utachukua eneo dogo tu la pori la akiba la Selou lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba elfu 50.
Amesema pori hilo ndilo kubwa miongoni mwa mapori ya aina hiyo ulimwenguni na ukubwa wake ni zaidi ya nchi za Rwanda na Burundi zikiunganishwa kwa pamoja.
Katibu mkuu amewataka wafanyakazi wa wizara na watanzania kwa ujumla kutokuwa kikwazo kwa utekelezaji wa mradi huo, na kwamba wadau wanaotaka kuisaidia Tanzania wasaidie kuhakikisha inatumia maliasili zake kupiga hatua ya kimaendeleo ikiwemo misaada ya teknolojia za kisasa na rafiki wa mazingira kusaidia kufikia malengo yake kimaendeleo.
Mfunzo hayo yaliyowashirikisha askari wa wanyamapori wapatao 98 kutoka Mamlaka ya wanayamapori Tanzania TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara ya Maliasili na utalii kwa askari wa wanyamapori na watumishi wengine wa wizara hiyo katika hatua za kuelekea mfumo wa jeshi usu.
