Hatimaye Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo CENI, imetangaza kwamba uchaguzi mkuu wa rais unaosubiriwa sana utafanyika Desemba 23 2018 na siyo Aprili 2019 kama ilivyotangazwa awali.
Tarehe hiyo imetangazwa baada ya ukosoaji mkubwa kwamba Rais Joseph Kabila, amekuwa akiahirisha uchaguzi mara kwa mara ili abaki anang’ang’ania madaraka.
CENI imetangaza tarehe hiyo siku chache baada ya balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley, kuonya uwezekano wa kuzuka vurugu ikiwa uchaguzi huo hautafayika haraka.
Hata hivyo, upinzani umesema haukubaliani na tarehe hiyo huku ukimtaka Rais Kabila kuondoka madarakani.
Uchaguzi mkuu ulipaswa kufanyika Desemba 2016 baada ya mihula miwili ya uongozi wa Kabila kumalizika, lakini umekuwa ukiahirishwa na alikataa kujiuzulu hali iliyoibua mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo.
