Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameitaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kubainisha tarehe za uchaguzi wa kitaifa, baada ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Desemba kuahirishwa kwa sababu za usalama.
Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa uongozini tangu 2001, alikataa kuachia madaraka baada ya kumalizika muhula wake wa pili Desemba mwaka jana, hatua iliyozusha maandamano yenye machafuko ambayo yamewaacha maelfu ya watu bila makazi katika mkoa wa Kasai.
Tangazo la jana, ambalo lilitolewa na kiongozi wa tume ya uchaguzi ya Congo – CENI, linakwenda kinyume na makubaliano ya kipindi cha mpito yaliyosimamiwa na Kanisa Katoliki mwishoni mwa mwaka jana kumzuia Kabila kugombea kwa muhula wa tatu.
Katika mahojiano yaliyochapishwa mwezi uliopita na gazeti la Ujerumani la Der Spiegel, Kabila amesema “hakuwa ameahidi chochote” katika makubaliano hayo ya Desemba.
