Mshukiwa mmoja ametambuliwa katika tukio la mlipuko uliotokea katika lango la shule ya chekechea mashariki mwa China wakati idadi ya vifo ikipanda hadi watu wanane.
Mlipuko huo ulitokea wakati jamaa za wanafunzi walikuwa wanawachukua kutoka shuleni watoto wao jana jioni.
Shirika la habari la Xinhua limesema polisi inachunguza mlipuko huo kama tukio la uhalifu na ikasema imemlenga mshukiwa mmoja ambaye haikutoa maelezo zaidi kumhusu.
Haijabainika kama mshukiwa huyo alikamatwa na hakuna ripoti iliyotolewa kuhusu lengo la mlipuko huo.
Aliyeshuhudia amenukuliwa na chombo cha habari akisema kulikuwa mtungi wa gesi uliokuwa kwenye duka moja la chakula kandoni mwa barabara ndio ulisababisha mlipuko huo.
Zaidi ya watu 65 walijeruhiwa na wanane kati yao wako katika hali mahututi.
