Muungano wa vyama vikuu vya upinzani nchini Kenya umetaja mgombea wake wa urais atakaepambana na Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa Agosti.
Muungano huo unaojulikana kama The National Super Alliance (NASA), ulimtangaza waziri mkuu wa zamani Raila Odinga kuwania nafasi ya rais, na makamu wa zamani wa rais Kalonzo Musyoka kuwa mgombea mwenza wake.
Odinga alisema ikiwa atachaguliwa atapambana dhidi ya rushwa, ambayo ni mmoja ya matatizo makuu yanayolikabili taifa hilo.
Kenyatta aliwashinda Odinga na Kalonzo mwaka 2013 kwa asilimia 50.07 ya kura, kukiwa na tofauti ya kura 4,099 kati yao, hali iliompelekea Odinga kupinga matokeo hayo mahakamani.
Kenyatta ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, na Odinga ni mtoto wa makamu wa kwanza wa rais Jaramogi Oginga Odinga.
