Mwanzilishi wa Jamii Forums akutwa na hatia, aachiwa kwa masharti

Mwasisi wa mtandao wa Jamii Forums nchini Tanzania, Maxence Melo amekutwa na hatia katika shtaka la kuzuia uchunguzi wa polisi hata hivyo ameachiwa kwa sharti la kutokutenda kosa kama hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Bwana Melo pamoja na mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums Mike Mushi walifuguliwa kesi yenye mashtaka mawili mwaka 2016 katika Mahakama ya Kisutu. Kosa la kwanza likiwa ni kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa kwa kikoa (domain) cha Tanzania (.tz) na shitaka la pili la kuzuia uchunguzi wa polisi kwa kutokutoa taarifa za waachama wawili wa mtandao huo waliodaiwa kuandika madai ya uhalifu kuhusu benki ya CRDB na Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa wakili wa wawili hao Bw Benedict Ishabakaki, Melo amekutwa na hatia ya shtaka la pili la kuzuia uchunguzi, huku Mike Mushi akikutwa hana hatia katika mashtaka yote mawili.

Exit mobile version