Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge, Bw. Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo ya ndani.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017) wakati akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.
Hata hivyo Alipopewa nafasi ya kujieleza, Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu uliopita, hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku miongoni mwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao.
Jana, mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na Serikali.
