Mwenyekiti wa bunge Mussa Azzan Zungu amewataka wabunge kujielekeza katika mjadala wa bajeti uliopo bungeni kwa sasa badala ya kutumia nafasi hiyo kuwashambulia viongozi wastaafu waliotumia nguvu na uwezo wao kuitumikia nchi hii.
Agizo la ZUNGU limefuatia baada ya baadhi ya wabunge kuanzia jana kuwataja marais wastaafu na kuwahusisha na masuala mbalimbali yanayoendelea katika sekta ya madini nchini huku wakitaka wachukuliwe hatua.
Akitoa angalizo hilo jana bungeni mjini Dodoma ZUNGU amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatoa kinga kwa rais aliye madarakani na hata rais mstaafu kushtakiwa au kufungua mahakamani shauri yoyote ya jinai dhidi yake.
Mwenyekiti huyo amesema mtu yoyote ambaye hatahusika katika sakata hilo, sio lazima kumtaja ndani ya bunge kwa kuwa atashughulikiwa na vyombo husika.
Agizo la ZUNGU limefuatia mwongozo ulioombwa na waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera,bunge,kazi,vijana,ajira na watu wenye ulemavu JENISTA MHAGAMA ambaye ametaka kujua kama ni sahihi kwa wabunge kuendelea kuwatuhumu marais wastaafu kwa kuwataka washtakiwe kuhusiana na suala la mchanga.
