
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imewaachia huru leo mchana vijana Jennifer Jovin (26), maarufu kama Niffer, na Mika Chavala, ambao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya uhaini.
Uamuzi huo umetolewa baada ya kesi yao kufikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, kwa ajili ya kutajwa. Wakati wa vikao vya Mahakama, Wakili wa Serikali, Titus Aron, aliwasilisha taarifa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu, hatarajii kuendelea na mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao, akitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Kufuatia maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Peter Kibala, alieleza kuwa hawana pingamizi dhidi ya hatua hiyo, akisisitiza kuwa mchakato huo unafuata taratibu za kisheria. Alisihi Mahakama kutoa tamko la kuwaachia huru washtakiwa.
Hakimu Lyamuya alikubali ombi la upande wa mashtaka na kutangaza kuwa Mahakama imewaachia huru washtakiwa wote wawili, isipokuwa endapo watakuwa wanahitajika kwa tuhuma nyingine tofauti na shauri hilo.