Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May leo Jumapili imesema kuwa mazungumzo yanaendelea na chama cha DUP katika kutafuta uungaji mkono wake kwa ajili ya kuunda serikali baada ya kusema mapema kuwa makubaliano yalikuwa yamefikiwa.
Chama cha Conservative cha waziri mkuu May kilipoteza viti vya wabunge wengi katika uchaguzi wa mapema siku ya Alhamisi na sasa kinahitaji msaada wa wabunge 10 kutoka chama cha DUP jambo linalozua wito kumtaka ajiuzulu.
Hapo jana May alilazimika kuwaachia wasaidizi wake wawili wa karibu baada ya kupata ugumu katika kuimarisha mamlaka yake kufuatia kushindwa kupata idadi kubwa ya wabunge katika uchaguzi huo.
Aidha Viongozi wakuu wa chama wameonya dhidi ya mabadiliko ya haraka ya uongozi wakisema kuwa yatasababisha usumbufu zaidi wakati huu Uingereza ikijiandaa kuanza mazungumzo ya kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya mapema tarehe 19 Juni.
