Nchini Uganda picha zinazomuonesha meya wa mji mdogo magharibi mwa nchi hiyo,Geoffrey Byamukama, akiwa amelazwa juu ya kitanda cha hospitali akionekana na majeraha katika magoti na vifundo vya miguu ,vilivyovimba pamoja na michubuko mahali pengine kwenye mwili wake, zilisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya ndani ya nchi siku ya Alhamisi.
Watetezi wa haki za binaadamu nchini humo wanasema picha hizo za mateso za mwanasiasa aliyewekwa kizuizini, akiwa na majeraha mwilini mwake, zinaonyesha ukatili wa kutojali unaofanywa na maafisa wa usalama nchini humo.
Idara ya usalama chini Uganda inakana kutumia mateso kama njia ya kupata ushahidi, kutoka kwa watuhumiwa waliowakamata.Msemaji wa polisi Asan Kasingye amesema maafisa wawili wa usalama wamekamatwa kuhusiana na mateso ya Byamukama lakini hakutoa maelezo zaidi.
Kasingye ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hawafumbii macho mateso na kwamba huo sio utaratibu wao wa kazi.
Byamukama alikamatwa April 5 kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji ya afisa wa polisi wa ngazi ya juu Andrew Felix Kaweesi, Machi 17.
