Polisi nchini Uganda imewakamata karibu watu 56 hapo jana kwa kuandaa mikutano ya hadhara kinyume cha sheria.
Wanaharakati waliingia mitaani kuupinga mpango wa serikali unaodai kuondoa ukomo wa umri kwa wagombea wa urais, ikiwa ni uwezekano wa kumwezesha Rais Yoweri Museveni ambaye ana umri wa miaka 72 kuendelea kuwa madarakani baada ya mwaka wa 2021.
Kwa sasa, katiba inawazuia raia wa zaidi ya umri wa miaka 75 kugombea wadhifa wa urais.
Maafisa wa upinzani wanalalamika kuhusu ukamataji huo, wakati pia wakiikosoa serikali kwa kuwakandamiza wapinzani wa mpango huo.
Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1986, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hana ufahamu wa mpango huo unaoweza kuurefusha utawala wake.
