Rais wa Russia Vladimir Putin amefutilia mbali mkutano wa waandishi wa habari kama ilivyo kawaida yake kila mwisho wa mwaka, ikiwa ni mara ya kwanza kutofanya hivyo katika muda wa muongo mzima.
Kama ilivyo desturi, kikao cha Putin na waandishi wa habari huchukua saa kadhaa na kimekuwa sehemu ya shughuli za putin katika kalenda ya kila mwaka ambapo huwa anajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, amewaambia waandishi wa habari kwamba kikao hicho cha habari cha kufunga mwaka, hakitafanyika bila kutaja sababu ambazo zimepelekea kikao hicho kutofanyika.
Peskov hata hivyo amesema kwamba Putin amekuwa akizungumza na waandishi wa habari kila mara, ikiwemo anapotembelewa na viongozi kutoka nchi nyingine, na kwamba kiongozi huyo wa Russia atapata fursa nyingine ya kuzungumza na waandishi wa habari.
