RAIS John Magufuli amepiga marufuku mpango unaopigiwa kelele na asasi ziziso za kiserikali, wa kutaka mwanafunzi anayejifungua kurudi shule, kwa maelezo kuwa mpango huo ni laana.
Amesisitiza kuwa kamwe katika kipindi cha uongozi wake, hataruhusu jambo hilo.
Akizungumza wakati wa kufungua barabara ya Bagamoyo – Msata, Rais Magufuli amesema serikali yake haiko tayari, kutoa Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kusomesha wazazi.
Badala yake, amesema serikali inatoa fedha hizo kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari wasome bure.
Ameagiza vyombo vya dola kwamba wakati msichana atabaki nyumbani kulea mtoto, wale wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi hao, wakafungwe miaka 30 ili nguvu alizotumia kumpa ujazito, akazitumie kuzalisha mali akiwa gerezani.
Katika suala hilo, Rais alisisitiza kuwa hata kama ni mtoto wake akipata ujauzito akiwa shule, kamwe hawezi kurudi shule.
Amezitahadharisha NGO kuwa makini na kunakili mambo ya kigeni kwamba watanakili na mambo ya ajabu, yakiwemo ya ushoga, licha ya kuwa wafadhili wa mambo hayo wanakuja na misaada.
