Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dk.John Pombe Magufuli amewasili jijini Mwanza jana jioni, na kuwaagiza watendaji wa serikali mkoani humo kuacha kuwabugudhi wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga katika maeneo yao kwani hata wafanyabiashara wakubwa walianza na mitaji midogo kama yao.
Rais magufuli ametoa agizo hilo akiwa njiani kuelekea Ikulu ndogo eneo la Capripoint muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mwanza, ambapo leo anatarajia kuzindua mradi mkubwa wa maji katika mji wa Sengerema uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 20 zilizotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na serikali ya Tanzania.
Kauli ya Rais Magufuli inakuja,wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wamachinga jijini Mwanza wanaodai kusumbuliwa na viongozi pamoja na watendaji wa halmashauri ya jiji la Mwanza,kufuatia kuwepo kwa mgogoro unaoendelea kufukuta uliosababisha wamachinga saba,wakiwemo baadhi ya viongozi wa muungano wa wamachinga mkoani humo kukamatwa na polisi.
